Thursday, November 18, 2010

Ghailani apatikana na hatia

Mshukiwa wa kwanza kutoka gereza  la Guantanamo Bay kushtakiwa katika mahakama ya kiraia nchini Marekani,  amepatikana na hatia ya kula njama ya kushambulia kwa bomu mali ya  taifa la Marekani.

Ahmed Khalfan Ghailani, raia wa Tanzania,  alishtakiwa kwa kosa la kuhusika katika mashambulizi ya kundi la kigaidi  la Al Qaeda, dhidi ya ubalozi wa Marekani nchini Kenya na Tanzania  mwaka 1998.

Viongozi wa mashtaka wamesema Ahmed Ghailani,  alichangia pakubwa katika maandalizi na mipango ya kundi la Al Qaeda ya  kulipua balozi za marekani nchini Kenya na Tanzania.

Watu 224 waliuawa kufuatia mashambulio hayo  mawili.
Mahakama hiyo ilifahamishwa kuwa Ghailani  alinunua mitungi ya gesi zilizolipuka pamoja la lori iliyobeba vilipuzi  hivyo.

Ghailani alikuwa anakabiliwa na mashataka 281  zikiwemo mauaji na jaribio la kuua.
Hatahivyo, Mahakama hiyo ilimpata bw Ghailani na  hatia moja pekee ya kupanga kuharibu mali na majengo ya serikali.

Ushahidi uliokuwa umewasilishwa mbele ya  mahakama hiyo ya Marekani dhidi ya mshukiwa huyo zimekataliwa na  mahakama kwa sababu zilikusanywa na maafisa wa ujasusi wa Marekani CIA,  katika magereza yasiyo rasmi nje ya Marekani kwa njia isiyofaa.

Maafisa hao wa ujasusi wanadaiwa kutumia mbinu  kali kumhoji mshukiwa huyo,ikiwemo kumtesa ili akiri mashtaka dhidi yake  na pia atoe habari zaidi.

Uamuzi huo wa mahakama unaonekana kuwa pigo  kubwa kwa utawala wa Rais Barack Obama, wa Marekani na ahadi yake ya  kuwafungulia mashtaka washukiwa wote wa ugaidi wanaozuiliwa katika jela  la Guantanamo Bay, katika mahakama ya kiraia.

Maafisa wa serikali ya Marekani sasa  wanachunguza upya jinsi ya kuendeleza kesi za washukiwa hao wa kigaidi,  na hivyo kumaanisha jela hilo la Guantanamo Bay, iliyoko Cuba huenda  isifungwe hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment